You are here

Je, Umormoni Ni Ukristo?

Printer-friendly version

Je, Umormoni Ni Ukristo?

Ufananisho wa Mormoni na Ukristo wa kihistoria.

Je, Umormoni ni Ukristo? Swali hili linaweza kuwa la kushangaza kwa wafuasi wa Mormoni na pia kwa baadhi ya wakristo. Wafuasi wa Mormoni watatambua ya kwamba wao huhusisha Biblia kama mojawapo ya vitabu vinne ambavyo wanavitambua kama Neno takatifu na pia kuamini Yesu Kristo ni jambo kuu katika imani yao kama inavyothibitishwa na jina lao rasmi la “Kanisa la Yesu Kristo wa Watakatifu wa Siku Hizi.” Zaidi ya hayo, wakristo wengi wameisikia kwaya ya kanisa la Mormoni ikiimba nyimbo za kikristo na wakapendezwa sana na jinsi dhehebu la Mormoni linavyoshikilia maadili/mafundisho mema ya hali ya juu na kuweko kwa familia zenye nguvu. Je, hii haidhibitishi ya kuwa kanisa la Mormoni ni la Kikristo?
 

"Kuweza kutatua swali hili vyema na kikamilifu, tunafaa kulinganisha mafundisho ya dini ya Mormoni na mafundisho ya Ukristo wa kihistoria na kibibli."

Kuweza kutatua swali hili vyema na kikamilifu, tunafaa kulinganisha mafundisho ya dini ya Mormoni na mafundisho ya Ukristo wa kihistoria na kibiblia. Kuwakilisha nafasi ya kanisa la Mormoni, tumetegemea vitabu vifuatavyo vya Mormoni na vinavyojulikana, vitatu vya kwanza ambavyo vimechapishwa na kanisa la Mormoni: Gospel Principles (1997), Achieving a Celestial Marriage (1976), na A Study of the Articles of Faith (1979) vilivyoandikwa na mfuasi wa Mormoni, James E. Talmage, na vilevile Doctrines of Salvation (nakala tatu) vilivyoandikwa na Rais wa kumi wa Mormoni na nabii Joseph Fielding Smith, Mormoni Doctrine (toleo la pili, 1979) kilichoandikwa na mfuasi wa Mormoni, Bruce R. McConkie na Mafundisho ya Nabii Joseph Smith.

1. JE, KUNA ZAIDI YA MUNGU MMOJA WA KWELI?

Biblia inafunza na vile vile wakristo (Orthodox) kutoka enzi za kale hadi sasa wameamini kuwa kuna Mungu mmoja tu wa kweli aishiye na hakuna Miungu wengine wowote (Kumbukumbu 6:4; Isaya 43:10,11; 44:6,8; 45:21,22; 46:9; Marko 12:29-34).

Tofauti na hayo, Kanisa la Mormoni linafunza ya kuwa kuna Miungu wengi (kitabu cha Ibrahimu 4:3 kuenda mbele), na kwamba twaweza kuwa miungu wa kike au wa kiume mbinguni, (Doctrine and Covenants 132:19-20; Gospel Principles uk. 245, Achieving a Celestial Marriage, uk. 130). Pia linafunza ya kwamba wale watakaohitimu kuwa miungu watapata watoto wa kiroho watakaowaabudu na kuwatolea zaka, kama vile tunavyomwabudu na kumtolea zaka Mungu Baba (Gospel Principles, uk. 302).

2. JE, MUNGU ALIWAHI KUWA BINADAMU KAMA SISI?

Tofauti na hayo, Kanisa la Mormoni linafunza kuwa Mungu Baba aliwahi kuwa binadamu kama sisi na kisha akaendelea akawa Mungu na ana mwili wa nyama na mifupa (Doctrine and Covenants 130:22; “Mungu mwenyewe alikuwa vile tulivyo na sasa ni mtu anayeheshimiwa zaidi na anakalia kiti cha utukufu mbinguni!” Kutoka kwa Mafundisho ya Nabii Joseph Smith uk. 345-347; Gospel Principles, uk. 9; Articles of Faith, uk. 430; Mormon Doctrine uk.321). Kwa kweli, Kanisa la Mormoni linafunza kuwa Mungu mwenyewe ana baba, babu na kadhalika (Mafundisho ya Nabii Joseph Smith uk. 373; Mormon Doctrine, uk. 577).

3. JE, YESU NA SHETANI NI NDUGU WA KIROHO?

Biblia inafunza na vile vile wakristo kutoka enzi za kale wameamini kuwa Yesu ni mwana wa pekee wa Mungu; amekuwa akiishi kama Mungu, ataishi milele na anasawiana na Mungu Baba (Yohana 1:1,14; 10:30; 14:9; Wakolosai 2:9). Huku akiwa hajawahi kuwa mdogo kuliko Mungu, wakati ulipofika aliweka kando utukufu aliogawana na Baba (Yohana 17:4,5; Wafilipi 2:6-11) na akafanywa binadamu kwa ajili ya ukombozi wetu; Kutwaa mwili kwake kunaonyeshwa jinsi mamake bikira alivyoshikishwa mimba na Roho Mtakatifu kwa njia inayopita akili na akamzaa (Matayo 1:18-23; Luka 1:34-35)

Tofauti na hayo, Kanisa la Mormoni linafunza kuwa Yesu Kristo ni ndugu wetu mkubwa aliyeendelea tu na kuwa Mungu, huku akiwa amezaliwa tu kama mtoto wa kiroho na mama na baba wa mbinguni, mimba ya Yesu Kristo ilipatikana baada ya kujuana kimwili kwa baba wa mbinguni na bikira Maria. (Achieving a Celestial Marriage uk. 129, Mormon Doctrine uk. 546-547,742). Maadili ya Mormoni husisitiza ya kwamba Yesu na Shetani ni ndugu (Gospel Principles, uk. 17-18; Mormon Doctrine, uk.192).

4. JE, MUNGU NI UTATU?

Biblia inafunza na vile vile wakristo kutoka enzi za kale wameamini kuwa Mungu Baba, Mwana na Roho Mtakatifu sio miungu tofauti au viumbe tofauti, mbali ni Mungu mmoja. Katika Agano Jipya, Mwana, Roho Mtakatifu na pia Mungu Baba wote wanatofautishwa na kujulikana kama Mungu. (Mwana: Marko 2:5-12; Yohana 20:28; Wafilipi 2:10-11; Roho Mtakatifu: Matendo 5:3,4; 2 Wakorintho 3:17,18; 13:14); Ilhali Biblia inafunza kuwa hawa watatu ni Mungu mmoja tu (angalia hoja 1).

Tofauti na hayo, Kanisa la Mormoni linafunza kuwa Baba, Mwana na Roho Mtakatifu ni miungu watatu tofauti, (Mafundisho ya Nabii Joseph Smith, uk. 370; Mormon Doctrine, uk. 576-577), na kwamba Mwana na Roho Mtakatifu ni watoto wa Baba na bibiye wa mbinguni (Joseph Fielding McConkie, Encyclopedia of Mormonism vol. 2, uk. 649).

5. JE, DHAMBI YA ADAMU NA HAWA ILIKUWA DHAMBI KUBWA AU BARAKA KUBWA?

Biblia hufunza na vile vile wakristo kutoka enzi za kale wameamini kuwa kutotii kwa wazazi wetu wa kwanza, Adamu na Hawa, kulikuwa dhambi kubwa. Kutokana na kuanguka kwao, dhambi iliingia duniani na kufanya watu wote kuwa wenye kulaumiwa na kuleta kifo. Hivyo basi tunazaliwa tukiwa wenye dhambi na tutahukumiwa kwa dhambi tunazozifanya kila mtu binafsi. (Ezekieli 18:1-20; Warumi 5:12-21).

Tofauti na hayo, Kanisa la Mormoni linafunza kuwa dhambi ya Adamu “ilikuwa hatua iliyohitajika kwenye mpango wa maisha na pia baraka kuu kwetu sisi wote.” (Gospel Principles, uk. 33, Kitabu cha Mormoni - 2 Nephi 2:25; Doctrines of Salvation vol. 1, uk. 114-115).

6. JE, TUNAWEZA KUJIFANYA KUSTAHILIKA MBELE YA MUNGU?

Biblia inafunza na vile vile wakristo kutoka enzi za kale wameamini kuwa mbali na kuokolewa na Yesu Kristo msalabani, sisi tumekufa kwa dhambi
(Waefeso 2:1,5) na hatuwezi kujiokoa sisi wenyewe. Kwa neema pekee, zaidi na matendo mazuri, Mungu anatusamehe dhambi zetu na anatufanya tustahili kuishi mbele zake (Waefeso 2:8-9; Tito 3:5-6). Sisi tunapaswa tujishikilie kwa Kristo kwa imani dhabiti. Hata hivyo, ni kweli kwamba kusipokuwepo na kubadilika kwa tabia ya mtu, basi ushuhuda wake wa imani kwa Kristo mpaka uchunguzwe; kuokolewa kwa neema pekee kufuatana na imani haimaanishi twaweza kuishi jinsi tunavyotaka (Warumi 6:1-4).

Tofauti na hayo, kanisa la Mormoni linafunza kuwa maisha ya milele mbele za Mungu (kama wanavyosema kuinuliwa kuishi mbinguni) lazima kupatikane tu kwa kutii amri za kanisa la Mormoni pamoja na tambiko zake za kipekee zote. Matendo yanahitajika kwa wokovu (kiingilio mbinguni). Gospel Principles, uk. 303-304; Pearl of Great Price – Hoja ya Tatu ya Imani; Mormon Doctrine uk. 339, 671; Kitabu cha Mormoni – 2 Nephi 25:23).

7. JE, KIFO CHA YESU KRISTO CHAWEZA KUWAFAIDISHA WALE WASIOMKUBALI

Bibilia inafunza na vile vile wakristo kutoka enzi za kale wameamini kuwa kusudi la Kristo kufa msalabani lilikuwa ni kutoa suluhisho kamili kwa dhambi za mwanadamu. Hata hivyo wale wasiokubali neema ya Mungu katika maisha haya hawatapata wokovu bali watahukumiwa na Mungu milele (Yohana 3:36; Waebrania 9:27; 1 Yohana 5:11-12).

Tofauti na hayo, kanisa la Mormoni linafunza kuwa kusudi la kifo cha Yesu Kristo msalabani lilikuwa ni kuleta ufufuo na kutokufa kwa watu wote, haijalishi kama wamemkubali kwa imani. Kifo cha Yesu Kristo msalabani sio kusudi la pekee la kupata ustahilifu na maisha ya milele bali mtu anafaa kutii amri za kanisa la Mormoni pamoja na tambiko za kipekee za kanisa hili (Gospel Principles, uk. 74-75; Mormon Doctrine, uk. 669).

8. JE, BIBLIA NI YA KIPEKEE NA NENO LA MWISHO LA MUNGU?

Biblia inafunza na vile vile Wakristo kutoka enzi za kale wameamini Biblia ni ya kipekee, neno la mwisho la Mungu, lisiloweza kukosa (2 Timotheo 3:16; 2 Waebrania 1:1,2; 2 Petero 1:21) na ambalo litasimama milele (1 Petero 1:23-25). Uwezo wa Mungu wa kuhifadhi maandiko ya Biblia ulidhihilishwa na ufumbuzi ya Vitabu vya Bahari ya Kifo (Dead Sea Scrolls).

Tofauti na hayo, kanisa la Mormoni linafunza ya kwamba Biblia imebadilishwa na kuharibiwa, imepoteza sehemu nyingi za muhimu sana na haina injili kamilifu. (Kitabu cha Mormoni – 1 Nephi 13:26-29; Doctrines of Salvation vol. 3 uk.190-191).

9. JE, KANISA LA MWANZONI LILIWAHI KUUWACHA KABISA UKRISTO?

Biblia inafunza na vile vile wakristo kutoka enzi za kale wameamini kuwa kanisa la kweli lilianzishwa na Yesu na hivyo basi halingeisha na halitaisha kamwe kutoka duniani. (Matayo 16:18; Yohana 15:16; 17:11). Wakristo wanatambua ya kwamba kumekuwa na wakati wa ufisadi na uchukizo katika Kanisa, lakini kumekuwa na wachache waliobaki na wakashikilia mahitaji muhimu ya kibiblia.

Tofauti na hayo, Kanisa la Mormoni linafunza kuwa kuna wakati ambapo kulikuwa na uchukizo kabisa wa kanisa kama lilivyoanzishwa na Yesu Kristo; na kwamba hali hii ya uchukizo “bado inaendelea isipokuwa tu kwa wale ambao wametambua injili iliyorejeshwa” ya Kanisa la Mormoni. (Gospel Principles, uk. 105-106; Mormon Doctrine, uk.44).

 



Hitimisho:

Hoja za hapo juu zilizomo kwenye italiki zinaonyesha injili ya kawaida inayoaminiwa na wakristo wa madhehebu yote kuanzia enzi za kale mpaka sasa. Kwa upande mwingine, dini zingine mpya kama vile Kimormoni zinajidai kuwa za kikristo lakini zinakubali maandiko mengine nje ya Biblia kuwa takatifu na kufundisha mafunzo mengine ya dini ambayo ni kinyume na Biblia, na zinaamini mafunzo mengine ya kigeni kabisa na yale ya Yesu Kristo na wafuasi wake.

Wamormoni wanakubaliana na Wakristo wengi juu ya baadhi ya adili muhimu zipatikanazo katika Biblia. Hata hivyo hoja zilizopo hapo juu ni baadhi ya mifano ya tofauti kubwa zilizoko kati ya ukristo kihistoria na kibiblia kwa upande mmoja na Umormoni kwa upande mwingine. Hata kama tofauti hizi haziwezi kutufanya tukose kuwa marafiki na Wamormoni, hatuwezi kuwachukulia kama ndugu na dada zetu katika Kristo. Biblia inatahadharisha dhidi ya manabii wa uongo watakaofundisha “injili nyingine” inayohusu “Yesu mwingine,” na walioshuhudiana na “roho mwingine” (2 Wakorintho 11:4,13-15; Wagalatia 1:6-9). Kulingana na ushahidi uliotolewa hapo juu, tunaamini kanisa la Umormoni husimamia tu injili kama hiyo isiyo ya kweli.

Imetajwa tayari ya kwamba ikiwa mtu atajidai kuwa mfuasi wa Mormoni na akane nguzo muhimu za Kimormoni – ya kwamba Joseph Smith alikuwa nabii wa Mungu, ya kwamba Kitabu cha Mormoni ni cha kweli na kiliandikwa na maongozi ya Mungu, ya kwamba wakati mmoja Mungu alikuwa mtu tu ambaye aliendelea na akawa Mungu kwa kufuata sheria na amri za kanisa la Mormoni, na kwamba kanisa la Mormoni lilianzishwa na Mungu – kanisa la Mormoni lingemkataa mtu kama huyu kujidai kuwa Mtakatifu wa siku hizi. Mtu hawezi kujiita mfuasi wa Mormoni ikiwa haamini maadili ya kidini yanayofunzwa na kanisa la Mormoni. Katika hali hiyo hiyo ikiwa kanisa la Mormoni haliwezi kuamini ukweli wa kibiblia ambao unaaminiwa na Wakristo wengine kutoka enzi za kale, Wakristo wataaminije Kimormoni kuwa Kikristo halisi?

Ikiwa Kanisa la Mormoni linaamini kuwa ndilo kanisa la kweli la kikristo la pekee, basi na lisijaribu kujionyesha waziwazi kuwa limo ndani ya jamii ya wakristo. Badala yake lafaa kuambia dunia nzima wazi wazi kwamba wale wanaojiita wakristo sio Wakristo kamwe na kwamba Kanisa la Mormoni ndilo kanisa la kweli la kikristo la pekee. Hili kwa kweli ndilo wanalofunzwa kisirisiri na sio hadharani.
 



TAARIFA ZA MADHEHEBU MATATU YA KIKRISTO JUU YA KIMORMONI.

Makanisa ya kikristo yanafunza juu ya imani kwa Mungu kuwa ni ya milele, Mungu ana uwezo wa maisha, hafi na hawezi kubadilika kwa matendo au maumbile. Katika miaka michache iliyopita, madhehebu kadhaa ya kikristo yamefanya utafiti juu ya mafunzo ya Kimormoni na kupata kuwa mafunzo yao yanayotofautiana sana na yale ya Kikristo ambayo yanatoka kwa Biblia.